ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Friday, June 7, 2013

LOWASSA: NINA WATU SI FEDHA


WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa (pichani) amesema hana fedha wala si tajiri bali ushawishi mkubwa alionao na wafuasi wengi wanaomuunga mkono katika shughuli za kimaendeleo ndivyo vinavyomng’arisha.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Akiba, Mikopo na Maendeleo Dodoma (Jamimado) katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Lowassa anayetajwa kuwa miongoni mwa wagombea urais mwaka 2015 kupitia CCM, ambaye amekuwa akiandamwa kwa kufanya siasa kwenye makanisa, alisema amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuchangia masuala ya maendeleo katika vikundi mbalimbali kwa lengo la kuwakwamua katika umasikini.
“Najua mmenipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Jumuiya ya Jumimado kwa kuwa mnajua ninachokifanya kwingine. Sina fedha, lakini nina ushawishi mkubwa kwa watu na wengi wananiunga mkono,” alisema.
Aliwataka wanajumuiya hiyo kujipanga ili wafanye harambee waweze kupata fedha zaidi ya sh milioni 500 na kwamba hilo linawezekana.
“Nataka tukifanya harambee iwe babu kubwa ili kila mtu ajue tumefanya nini, na nilitamani tufanye harambee hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu. Unajua ukiwawezesha akina mama umeliwezesha taifa na utakuwa umeondoa umasikini,” alisema.
Lowassa alisema ameamua kutoa sh milioni 10 kwa ajili ya maandalizi ya harambee itakayokuwa na tija pamoja na kuutunisha mfuko wa jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Aksa Lemwayi katika risala yake alimmwagia sifa lukuki Lowassa kuwa wanamtambua ni baba wa kupinga umasikini katika maeno mbalimbali hapa nchini.
“Tunatambua jinsi anavyosimamia na kutekeleza maamuzi yake katika shughuli za kimaendeleo, amekuwa ni kiongozi wa aina yake katika kutambua na kuthamini shughuli za maendeleo katika jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa Lowassa amekuwa ni kiongozi anayepigana kufa au kupona kuhakikisha jamii inaondoka kwenye lindi la umasikini.
Lemwayi alisema wanajisikia furaha na ufahari kumualika Lowassa kwenye uzinduzi wa jumuiya hiyo.
Alisema kuwa jumuiya hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto za kukosekana kwa usafiri kwa wanachama wanaotoka maeneo mbalimbali nje ya mji.
Alibainisha kukosekana kwa usafiri kunafanya shughuli za jumuiya hiyo ikiwemo vikao vya mara kwa mara kushindwa kutofanyika au kufanyika kwa wakati usiostahili.
Lemwanyi aliziomba taasisi za kifedha zipanue mitandao katika kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha Watanzania wengi kujikwamua katika dimbwi la umasikini ambao kwa sasa ni kilio kikubwa kwa wananchi wengi.
na Danson Kaijage, Dodoma - TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...